read

Aya 185-186: Kila Nafsi Itaonja Mauti

Kila nafsi itaonja mauti.

Ni glasi inayozunguka kwa kila mtu, awe mwema au muovu mfalme au kabwela. Haiwezekani wala hakuna njia yoyote ya kuyakimbia mauti. Lile wanalofikiria madaktari ni kujaribu kurefusha maisha ya mtu tu, sio kukinga mauti. Jaribio la mwisho walilifanya madaktari la kurefusha maisha mwaka 1967, ni kupachika moyo mwengine wa mtu anayekaribia kufa, anatolewa moyo na kuwekwa kwa mwenye moyo mgonjwa baada ya kutolewa.

Lakini jaribio hili halikufanikiwa, ingawaje lilifanyika mara kwa mara. Kukawa na mzozo kwa madaktari wakubwa wakasema hilo ni kosa lisilosameheka. Kwa sababu haiwezekani kuhakikisha kuwa yule anayetolewa moyo kweli angekufa baada ya muda mfupi? Kwani kifo hutokea kwa namna tofauti; kama vile kuzimia muda mrefu na kukosa kuvuta pumzi, wala hakuna njia ya kujua hali hii baina ya kifo na uhai. Mara ngapi madaktari wamethibitisha kifo, kisha wagonjwa wakarudiwa na uhai.

Jana nimesoma katika gazeti moja kwamba kikongwe mmoja Mmisri alizimia, watoto wake wakaita madaktari, wakathibitisha bila ya wasiwasi kwamba amekufa, baada ya kutangaza kifo, kutoa matangazo ya tanzia, kuchimba kaburi na watu kuhudhuria mazishi, alifungua macho yake na akawaambia watu waliokuja: "Nendeni kwenye shughuli zenu Mungu awalipe."

Ikiwa madaktari wameshindwa kuurefusha umri wa mtu na hata kumjua kama amekufa au ni mzima, basi kumkinga na mauti ndio hawawezi kabisa.

Bila shaka mtatekelezewa malipo yenu siku ya kiyama.

Hakuna malipo duniani kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) isipokuwa mtu atal- ipwa malipo kamili siku ya kiyama.

Wafasiri wengi wamesema kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) humpa mtu sehemu ya malipo ya amali yake baada ya mauti kabla ya Kiyama, kisha humalizia malipo yake Siku ya Kiyama. Kwa hivyo hapo ndipo unatimia utekelezaji kwa ukamilifu. Na wamedai kuwa neno Tuwaffauna linafahamisha hilo.

Ama sisi hatufahamu neno hilo zaidi ya lilivyoelezwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu. "Na hakika sisi tutawatekelezea fungu lao bila ya kupunguzwa." (11:109). Kauli hii haifahamishi kugawanywa, si kwa mbali wala karibu. Ndio, iko Hadith isemayo: "Hakika kaburi ni bustani katika mabustani ya pepo au ni shimo katika mashimo ya moto." Lakini hili ni jambo jengine na kufahamisha kugawanywa malipo ni jambo jengine.
Mwenye kuepushwa na moto akatiwa peponi basi huyo amefuzu.

Bali hata mwenye kuepushwa na moto na asitiwe peponi pia atakuwa amefuzu. Wanafalsafa wengi wamepanga kuwa 'kutokuwa na maumivu ni raha' na 'kutokuwa na uovu ni wema'

Na hayakuwa maisha ya dunia ila ni starehe idanganyayo.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesifu kuwa ni starehe inayohadaa, kwa vile mtu ana- hadaika nayo, au kwa sababu mtu akimiliki kitu basi inatokea kujidanganya. Imam Ali (as) anasema: "Dunia inadhuru, inadanganya na inapita."

Kwa hakika mtapata misuko suko katika mali zenu na nafsi zenu, na mtasikia udhia mwingi kutoka kwa wale waliopewa Kitabu kabla yenu na kwa washirikina.

Hii ndiyo thamani ya haki na pepo. Ni mapambano machungu pamoja na wabatilifu, ni subira kutokana na tuhuma zao na uzushi wao, na kujitolea mhanga kwa nafsi na mali. Kadiri mtu anavyokuwa na nguvu katika dini yake ndivyo mitihani yake inavyozidi na kuwa mikubwa.

Hilo ni kwa kwa sababu umuhimu wa watu wa haki unaleta machukivu kwa wabatilifu, kwani hakuna kupatana wala kupakana mafuta baina ya haki na batili. Watu wa batili walikuwa na bado ni wengi na wenye nguvu. Nao hawawezi kuwanyamazia maadui zao katika itikadi na misingi. Ni nani ajuaye kuwa unambughudhi na kumchukia, kisha akukubalie na kukunyamazia? isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mola wako?

Kwa sababu hiyo ndipo ikawa historia ya Mitume na viongozi wazuri ni ya vita na jihadi pamoja na washirikina na wafisadi. Ama mitihani ya nafsi na mali na mengi- neo ni natija ya kila vita.

Makusudio ya wale waliopewa Kitabu kabla yenu ni mayahudi na manasara. Na waliofanya ushirikina ni Warabu waliotangaza vita na Mtume

Na mkisubiri kutokana na jihadi ya wabatilifu na misukosuko inayowapata na mkiogopa Mwenyezi Mungu katika yanayopasa kumwogopa, basi hayo ya kuwa na subira kutokana na misukosuko na kuogopa yaliyoharamishwa, ni miongoni mwa mambo ya kuazimia.

وَإِذْ أَخَذَ اللَّهُ مِيثَاقَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ لَتُبَيِّنُنَّهُ لِلنَّاسِ وَلَا تَكْتُمُونَهُ فَنَبَذُوهُ وَرَاءَ ظُهُورِهِمْ وَاشْتَرَوْا بِهِ ثَمَنًا قَلِيلًا ۖ فَبِئْسَ مَا يَشْتَرُونَ {187}

Na Mwenyezi Mungu alipochukua ahadi na wale waliopewa Kitabu, lazima mtakibainisha kwa watu wala hamtakificha. Wakakitupa nyuma ya migongo yao na wakakiuza kwa thamani ndogo. Basi ni mabaya waliyoyauza.