read

Aya 113 -115: Wote Si Sawa

Lugha

Mwenye Majmaul-bayan anasema: Tofauti kati ya neno Sura’ na A’jala ni kwamba Sura’ ni kufanya haraka linalojuzu kufanywa. Nako kunasifiwa. Na A’jala ni kufanya haraka jambo lisilofaa kufanywa, nako kunashutumiwa.

Maana

Aya hizi tatu ziko wazi hazihitaji tafsir. Maana yake kwa ujumla ni kwamba watu wa Kitabu hawako sawa kwamba wote wamepotea, bali wako watu wema miongoni mwao. Wafasiri wengi wamechukulia sifa hii kwa aliyesilimu miongoni mwa watu wa Kitabu, na uzuri wa uislamu wake kimatendo na kiitikadi.

Hukumu Ya Mwenye Kuacha Uislamu

Mwito wa kumwamini Muhammad kama Mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa watu wa ulimwenguni bado upo mpaka Siku ya Mwisho. Nao unaelekezwa kwa watu wote, wa Mashariki na Magharibi. Mwenyezi Mungu anasema: "Sema : Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu nyote …" (7:158).

Dalili ya ukweli wake ni mantiki ya kiakili, kuthibiti muujiza na kufaa dini kwa maisha. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) anasema: "Msingi wa dini yangu ni akili."

Na Mwenyezi Mungu anasema katika Kitabu chake Kitukufu: "Enyi ambao mmeamini muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume (wake) anapowaitia katika yale yatakayowapa maisha” (8:24)

Lengo letu sio kutoa dalili za Utume wa Muhammad (s.a.w),1 isipokuwa lengo ni kubainisha kuwa je, asiyeamini Utume wa Muhammad anastahili adhabu: au hapana budi ya ufafanuzi?

Kabla ya kumtofautisha mjuzi na asiye mjuzi na asiyemudu na mzembe, tutaonyesha msingi na vipimo vya kwanza vya kustahili adhabu au kutostahili; kutokana na hivyo, uhakika utafumbuka na kuwapambanua watu.

Wote wameafikiana kwamba mtu, vyovyote awavyo, dini yoyote aliyo nayo, hastahili adhabu ila baada ya kusimamishiwa hoja. Na hoja haisimami ila baada ya kuweza yeye kufikia kwenye dalili ya haki na kuweza kwake kuitumia. Hapo akiacha hatakuwa na kisingizio.

Ikiwa hakupata dalili ya haki yenye msingi au aliipata akashindwa kuifikia au aliifikia na akatekeleza mtazamo wake wa haki mpaka akafikia mwisho, lakini pamoja na hayo haki haikumdhihirikia, basi yeye atakuwa na udhuru, kwa sababu ya kutokamilika hoja juu yake.
Kwa sababu, asiyethibitikiwa na haki haadhibiwi kwa kuiacha, ila ikiwa amezembea katika utafiti.

Vile vile miongoni mwa kawaida za msingi ambazo zinaambatana na utafiti huu ni ile ya "Adhabu kuepukwa na mambo yenye kutatiza."

Kwa hiyo haijuzu kumhukumu mwenye kuiacha haki kuwa ni mwenye makosa anayestahili adhabu, maadamu tunaona kuwa kuna uwezekano kuwa anao udhuru katika kuacha kwake. Na kawaida hii inafungamana na watu wote, sio waisla- mu tu. Pia inakusanya aina zote za mipaka.

Mfano kawaida ya 'Mwenye kukosea katika ijtihadi, basi kosa lake linasamehewa'. Kawaida hii ni ya kiakili, haiwezekani kuihusisha na dini fulani tu, madhehebu, shina au tawi. Baada ya maelezo hayo hebu tuangalie hali hizi zifuatazo:

1) Kuishi binadamu mji ulio mbali na uislamu na waislamu; wala hakufikiliwa na mwito au hata kusikia jina la Muhammad (s.a.w) katika maisha yake yote. Pia awe hajawaza kwa karibu au mbali kwamba duniani kuna dini yenye jina la kiislamu na Mtume aitwaye Muhammad (s.a.w). Hapana mwenye shaka kwamba huyu atasamehewa kwa kuwa hastahili adhabu. Maana akili ina hukumu ubaya wa adhabu bila ya ubainifu na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na sisi si wenye kuadhibu mpaka tupeleke Mitume." (17:15)

Bila shaka akili ni Mtume wa ndani kwa ndani, ila tu yenyewe ni dalili ya kupatikana Mwenyezi Mungu tu. Ama dalili ya kuthibiti Utume wa Mtume, hapana budi kuwako na muujiza na udhihirishwe na yeye mwenyewe pamoja na akili kuhukumu kutowezekana kudhihiri kwa wasiokuwa Mitume.

2) Kuusikia mtu uislamu na Muhammad, lakini akawa hawezi kupambanua haki na batili, kwa sababu ya kushindwa kwake na kutoweza kufahamu dalili za haki na maarifa yake. Huyu pia anasamehewa. Kwa sababu yeye ni sawa na mtoto au mwenda wazimu. Mfano ni akitomwamini Muhammad (s.a.w) tangu udogo kwa kuwafuata wazazi wake na akajisahau alipokuwa mkubwa, akaendelea na itikadi yake bila ya kuitilia shaka yoyote, huyu atasamehewa. Kwa sababu kumkalifisha aliyejisahau asiye na uwezo ni sawa na kumkalifisha aliyelala. Amesema Muhaqqiq Al-Qummi: "Kujikomboa kutokana na kuiga wazazi ni jambo lisilofikiriwa na wengi, bali hata linakuwa zito aghlabu kwa wanavyuoni walioto- sheka ambao wanadhani kuwa wamejivua kutokana na kuiga huko." Amesema tena: "Asiyeweza kung'amua wajibu wa kujua misingi, ni sawa na mnyama na mwedawazimu ambao hawana taklifa yoyote."

Sheikh Tusi anasema: "Mwenye kushindwa kupata uthibitisho yuko katika daraja ya mnyama."

Hata hivyo, ikiwa aliyejisahau atakumbushwa wajibu wa maarifa, au kuambiwa na mtu: "Wewe uko au hauko sawa katika itikadi yako", lakini pamoja na hayo akang'ang'ania na wala asifanye utafiti na kuuliza, basi huyo atakuwa ni mwenye dhambi, kwa sababu atakuwa ni mzembe, na kutojua kwa mzembe si kisingizio.

3) Kutomwamini Muhammad (s.a.w) pamoja na kuwa anao uwezo wa kutosha wa kufahamu haki, lakini yeye alipuuza wala asijali kabisa: au alifanya utafiti pungufu na akauacha bila ya kuangalia mwisho wake; kama wafanyavyo wengi, hasa vijana wa kisasa. Basi huyu hatasameheka kwa sababu amekosea bila ya kujitahidi na alikuwa na uwezo wa kujua haki, lakini akapuuza. Ni wazi kuwa pia ataadhibiwa ambaye amefanya utafiti na akakinai, lakini pamoja na hayo akakataa kumwamini Muhammad (s.a.w) kwa ubaguzi na mali.

4) 4).Kuangalia dalili na kuwa na mwelekeo wa kufuata haki kwa ikhlasi, lakini pamo- ja na hayo akakosa kuelekea kwenye njia ambayo itamwajibishia kumwamini Muhammad (s.a.w) ama kwa kushikamana kwake na mambo yenye kutatiza ya ubatilifu bila ya kuangalia ubatilifu wake, au kuchanganyikiwa na mengineyo ambayo yanazuia kuona haki. Huyu ataangaliwa hali yake, ikiwa atakanusha Utume wa Muhammad (s.a.w) kwa kauli ya mkato, basi yeye ataadhibiwa na kustahili adhabu.

Kwa sababu yule ambaye imefichika kwake haki, haifai kwake kukataa moja kwa moja kukanusha haki. Inawezekana kuwa haki ipo lakini akazuiliwa, kuifika, na aghlabu huwa hivyo, kwa sababu mambo ya ulimwenguni yapo lakini tuyajuayo ni machache tu. Hali ni hivyo hivyo kuhusu kuwajua Mitume na wasuluhishi. Ni nani awezaye kujua kila kitu?

Watu wa mantiki wamelielezea hilo kwa ibara mbali mbali, miongoni mwazo ni: Kutokujua hakumaanishi kutokuwepo, kutopatikana hakumaanishi kuacha kupatikana, kuthibitisha na kukanusha kunahitaji dalili.

Tumewaona wanavyuoni wengi wakiungana na hakika hii. Wanazituhumu rai zao na kujichunga katika kauli zao; wala hawajifanyi kuwa wao ndio kipimo cha ukweli. Hawawezi kusema: "Rai hii ni takatifu isiyo na shaka, na nyinginezo si chochote." Bali wao huipa mtazamo wa kujiuliza kila rai. Dalili kubwa zaidi ya kuwa mtu hana elimu, ni kule kujidanganya mwenyewe, kuiona safi elimu yake, na kudharau rai na itikadi za wengine.

Zaidi ya hayo kuacha kukinai mtu mmoja miongoni mwa watu kuhusu Utume wa Muhammad (s.a.w) hakumruhusu kukanusha Utume wa Mtume Mtukufu (s.a.w) moja kwa moja. Na kama akifanya hivyo, basi atakuwa na jukumu.

Hasa baada ya kuona idadi ya mabingwa ambao hawakuathiriwa na kurithi au mazingira, wakimwamini Muhammad na risala yake; si kwa lolote isipokuwa kuiheshimu haki na kuikubali hali halisi ilivyo.2

Hayo ni ikiwa atapinga. Ama akiangalia dalili wala asikinai na pia asipinge; wakati huo huo akawa amenuia kwa moyo safi kuiamini haki wakati wowote itakapomdhihirikia; kama vile mwanafiqh mwadilifu ambaye hufutu jambo kwa nia ya kubadilisha mara tu ikimbainikia kuwa amekosea, basi huyu hatakuwa na jukumu, kwa sababu mwenye kukosea katika ijtihadi yake bila ya kufanya uzembe, hataadhibiwa kwa kukosea kwake; kama inavyohukumu akili na maandishi pia.

Imepokewa kutoka kwa Imam Jafar Sadiq (a.s.), amesema: "Lau kama watu wasipofahamu (jambo) wakasimama na wala wasipinge, basi hawakukufuru…" Katika Riwaya nyingine: "Hakika anakufuru tu akipinga …"

Sheikh Ansari katika kitabu chake maarufu Arrasil mlango wa Dhana katika Usul, anasema: "Hadith nyingi zimefahamisha kuthibiti ukati na kati baina ya kufuru na imani." Ya kwamba mpingaji ni kafiri, mwenye kuitakidi ni Mumin, na mwenye shaka si kafiri wala Mumin.

Katika Hadith zinazowezekana kuzitolea dalili ya kutoadhibiwa mwenye kufanya ijitihadi bila ya uzembe kama akikosea katika mambo ya itikadi, ni Hadith hii mashuhuri kwa sunni na shia:

"Akijitahidi hakimu na akapata basi atalipwa mara mbili. Na akijitahidi akakosea, basi atalipwa mara moja."

Kama mtu akisema kuwa Hadith hii inahusu mwenye kujitahidi katika matawi si katika masuala ya itikadi, kama walivyodai baadhi ya wanavyuoni, basi tutamjibu hivi: Linalomlinda, mwenye kujitahidi katika hukumu, asiadhibiwe ni kule kujichunga kwake na kutofanya uzembe katika utafiti. Na kinga hii inapatikana hasa katika masuala ya kiitikadi.

Zaidi ya hayo Mafaqihi wote wameafikiana kwa kauli moja kwamba mwenye kushindwa kuifikia itikadi ya kweli, anasamehewa. Miongoni mwao ni wale waliohusisha Hadith hii na matawi. Nasi hatuoni tofauti yoyote kati yake na yule mwenye kujitahidi, aliyetoa juhudi zake. Kwa sababu, wote wawili wameshindwa kujua maadam hawakuufikia uhakika.
Kwa ufupi ni kwamba mwenye kuipinga, haki yoyote, basi ataadhibiwa, ni sawa awe amejitahidi au la, isipokuwa kama hana maarifa, kama mnyama. Kama akibakia kwenye msimamo wa kutopinga wala kuthibiti sawa, kujitahidi na kuangalia dalili au alifanya ijtihadi pungufu, basi ataadhibiwa. Ikiwa ameangalia dalili akajitahidi mpaka akafikia mwisho wake, basi yeye atasamehewa kwa sharti ya kubakia na mwelekeo wa haki kwa kuazimia kubadili msimamo wake wakati wowote itakapomdhihirikia haki.

Unaweza kuuliza: Umesema kuwa mwenye kushindwa kujua itikadi ya kweli - kama vile Utume wa Muhammad - atasamehewa. Vile vile mwenye kujitahidi ambaye hakuzembea katika jitihadi. Je, maana yake ni kuwa inajuzu kwetu kufanya naye muamala wa kiislamu, kama kuoa, kurithi n.k.

Jibu: Msamaha tunaoukusudia hapa ni kutostahiki adhabu akhera; ama kuoa na kurithi hapa duniani ni jambo jengine. Na kila asiyeamini utume wa Mtume Muhammad (s.a.w) kwa hali yoyote atakayokuwa, haifai kuwa na muamala naye wa kiislam k.v. ndoa, urithi n.k. Ni sawa awe kesho atapona au ataangamia; kama ambavyo mwenye kusema "Laila ilaha illa llah Muhammad Rasulullah" anastahiki ya waislamu, ni juu yake yaliyo juu yao, hata kama alikuwa ni fasiki, bali hata mnafiki vile vile.

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا لَنْ تُغْنِيَ عَنْهُمْ أَمْوَالُهُمْ وَلَا أَوْلَادُهُمْ مِنَ اللَّهِ شَيْئًا ۖ وَأُولَٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۚ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ {116}

Hakika wale ambao wamekufu ru, haitafaa kitu mali yao wala watoto wao kwa Mwenyezi Mungu, na wao ndio watu wa motoni, wao humo watadumu.

مَثَلُ مَا يُنْفِقُونَ فِي هَٰذِهِ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا كَمَثَلِ رِيحٍ فِيهَا صِرٌّ أَصَابَتْ حَرْثَ قَوْمٍ ظَلَمُوا أَنْفُسَهُمْ فَأَهْلَكَتْهُ ۚ وَمَا ظَلَمَهُمُ اللَّهُ وَلَٰكِنْ أَنْفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ {117}

Mfano wa wanavyovitoa katika maisha haya ya dunia ni kama mfano wa upepo wenye baridi kali uliofikilia shamba la watu waliodhulumu nafsi zao, ukaliangamiza. Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, lakini wanajidhulumu wenyewe.
  • 1. Tumeonyesha dalili hizo tulipofasiri Sura Baqara Aya23 - 25. Vile vile tutataja sehemu ya hulka za Mtume (s.a.w) katika kufasiri Aya160 ya Sura hii tuliyonayo (Al-Imran).
  • 2. Miongoni mwao ni Leopold Fais Mu-Austria ambaye alijiita Muhammad Asad, na akatunga kitabu Al- Islam ala muftariq turuq. Mwengine ni Vaglire mwenye kitab Difa anil-Islam, na wengineo ambao majina yao siyajui. Nimesikia kuwa kuna Mwirani mmoja ameandika kitabu maalum cha majina ya watu wa ki-magharibi waliosilimu nao ni wengi.