read

Aya 105-109: Kuhitalifiana Baada Ya Mtume

Maana

Wala msiwe kama wale waliofarakana wakahitalifiana baada ya kuwajia wao dalili zilizo wazi.`

Aya hii inamalizia kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote …"

Makusudio ya wale waliofarakana ni watu wa Kitabu. Ambapo mayahudi walichangukana vikundi sabini na moja baada ya Mtume wao Musa wakristo wakawa vikundi sabini na mbili baada ya Mtume wao Isa. Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu. "Baada ya kuwajia hoja iliyo wazi," inafahamisha kwamba mtu haadhibiwi kwa kuiacha haki na kufuata batili, ila baada ya kubainishiwa hoja.

Ama siri ya mkazo huu na kuupa kipaumbele muungano wa umma, ni kuwa utengano ndio kiini cha ufisadi na kwamba umma uliotengana hauwezi kuwa na maisha mazuri, wachilia mbali kuuita umma mwingine kwenye kheri.

Pamoja na kuwapo Riwaya nyingi, na Hadith zinazohimiza muungano wa waislamu, lakini bado wamefarakana na kuwa vikundi mbali mbali, wamewazidi mayahudi kwa vikundi viwili zaidi na wakristo kikundi kimoja; kama ilivyoelezwa katika Hadith mashuhuri.

Kuna Hadithi nyingine isemayo: "Mtakuwa na desturi ile ile ya waliokuwa nayo kabla yenu."

Akaulizwa: "Unakusudia mayahudi na manaswara ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?" Akasema: "Kumbe ninawakusudia kina nani? Utachanguka uthabiti wa waislamu."

Katika kitabu Al-Jam'u Bainas-Sahihayni cha Hamid, kwenye Hadith Na. 131, anasema: Katika yaliyoafikianwa kutoka Musnad ya Anas bin Malik, amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w): "Watanijia watu miongoni mwa sahaba zangu kwenye hodhi, nitakapowaona na watakapokuwa wanaletwa kwangu watazuiwa ili wasinifikie. Hapo nitasema: 'Ewe Mola! Sahaba zangu, sahaba zangu!' Nami nitaambiwa: 'Wewe hujui walizua nini baada yako.'"

Katika kitabu hicho hicho Hadith Na. 267 anasema: "Katika yaliyaofikianwa kutoka Musnad ya Abu Huraira kutoka katika njia mbali mbali, ni kwamba Mtume amesema: "Wakati nikiwa nimesimama - siku ya Kiyama - litatokea kundi la watu mpaka nitakapowatambua, atatokea mtu baina yangu na yao na awambie: 'Haya twendeni.' Mimi nitauliza: Mpaka wapi? Naye aseme: 'Mpaka motoni.' Nami niulize wana nini? Naye ajibu: 'Hakika wao walirtadi baada yako.'"

Siku ambayo nyuso zitang'aa na nyuso (nyingine) zitasawijika.

Makusudio ya Siku, ni Siku ya Kiyama. Kung'aa uso, ni fumbo la kuonyesha fura- ha ya mumin kufurahia radhi za Mwenyezi Mungu na fadhila Zake. Kusawijika uso ni huzuni ya kafiri na fasiki kwa ghadhabu na adhabu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu
.
Na ama ambao nyuso zao zitasawijika, (wataambiwa) "je, mlikufuru baada ya kuamini kwenu?"
Arrazi, Tabari na wafasiri wengine wengi wamenukuu kutoka kwa baadhi ya waliopita, kwamba makusudio ya watakaoambiwa hivyo ni Khawariji. Kwa sababu Mtume alisema kuwahusu: "Hakika wao watachomoka kutoka katika dini, kama unavyochomoka mshale kutoka katika uta (upinde)." Lakini dhahiri ya Aya inamkusanya kila mwenye kukufuru baada ya imani, wakiwemo Khawariji, watu wa bid'a na wenye maoni potofu. Kwa vile adhabu haihusiki tu na aliyekufuru baada ya imani bali inamuhusu kafiri yeyote, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Onjeni adhabu, kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyakanusha. Na ama ambao nyuso zao zitang'aa, watakuwa katika rehema ya Mwenyezi Mungu, wao humo watadumu.

Rehma ya Mwenyezi Mungu ni Pepo. Kwa ufupi ni kwamba wale ambao wameshikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu, na kufanya mambo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na wakasaidiana kwenye mambo ya kheri na ya masilahi ya umma, basi watafufuliwa kesho wakiwa watukufu, wenye furaha na wenye kuridhia.

Ama wale ambao wamehitalifiana kwa kuipupia dunia, wasiojishughulisha na dini wala umma au nchi, na ambao hawajishughulishi na lolote isipokuwa masilahi yao na ya watoto wao tu, basi wao watafufuliwa Siku ya Kiyama wakiwa madhalili, wenye hasara na makazi yao ni Jahanam, nayo ni marejeo mabaya kabisa.

Ajabu ya maajabu ni kwamba baadhi ya wenye nyuso zilizosawijika wanadai kuwa wanamzungumzia Mungu na kutumia Jina lake, lakini mtu akiwaambia "Muogopeni Mungu" wao husema: "Umemkufuru Mwenyezi Mungu."Aliyewatangulia katika hilo ni Abdul Malik bin Marwan aliposema pale alipochukua Ukhalifa: "Kuanzia leo atakayeniambia muogope Mwenyezi Mungu nitamkata kichwa chake."

Hizo ni Aya za Mwenyezi Mungu, tunakusomea wewe kwa haki.

Hizi, ni ishara ya Aya zinazoelekezea kuneemeshwa watu wema na kuadhibiwa makafiri. Msemo unamwelekea Muhammad (s.a.w), muulizaji anaweza kuuliza: "Kuna faida gani katika habari hii, ikiwa Muhammad anajua kwa yakini kwamba Aya hizi ni haki na ni kweli?"

Jibu: Ni kawaida ya Qur'an kulikariri hilo katika Aya kadhaa. Na makusudio sio kwa Muhammad hasa, bali ni kwa yule anayetia shaka na kudhani kwamba Aya hizi na mfano wake zinatoka kwa Muhammad, si kwa Mwenyezi Mungu.

"Na hukuwa mwenye kusoma kitabu chochote kabla ya hiki wala hukukiandika kwa mkono wako wa kuume, ingekuwa hivyo wangefanya shaka wabatilifu." (29:48)

Na Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu viumbe.

Kwa sababu dhuluma ni mbaya na Mwenyezi Mungu ameepukana nayo. Aya hii ni dalili ya mkato kwamba Mwenyezi Mungu hakalifishi mja asiloliweza.

كُنْتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنْكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ ۗ وَلَوْ آمَنَ أَهْلُ الْكِتَابِ لَكَانَ خَيْرًا لَهُمْ ۚ مِنْهُمُ الْمُؤْمِنُونَ وَأَكْثَرُهُمُ الْفَاسِقُونَ {110}

Mmekuwa ni umma bora mliotolewa kwa watu, mnaamrisha mema na kukataza maovu na mnamwamini Mwenyezi Mungu. Na lau watu wa Kitabu wangeliamini ingekuwa heri kwao. Katika wao kuna wanaoamini na wengi wao ni wafasiki.

لَنْ يَضُرُّوكُمْ إِلَّا أَذًى ۖ وَإِنْ يُقَاتِلُوكُمْ يُوَلُّوكُمُ الْأَدْبَارَ ثُمَّ لَا يُنْصَرُونَ {111}

Hawatawadhuru isipokuwa kuwaudhi tu, na wakipigana nanyi watawakimbia, kisha hawatasaidiwa.