read

Aya 1: Amewaumba Kutokana Na Nafsi Moja

Lugha

Neno Zawj lina maana ya aliye na mwengine wa jinsi yake (jozi). Kwa hiyo mwanamke aliyeolewa ni jozi na mume aliyeoa ni jozi.

Maana

Katika Aya hii kuna mambo yafuatayo:

Enyi Watu! Mcheni Mola Wenu.

Imesemekana kuwa msemo unawahusu watu wa Makka tu. Lakini ilivyo hasa ni kuwa unawaenea wote wanaokalifiwa na sharia. Kwa sababu dhahiri ya neno inawakusanya wote, wala hakuna dalili yoyote ya kuhusisha. Bali amri ya kumcha Mwenyezi Mungu inatilia mkazo kuwa inawaenea wote. Kwa sababu, wajibu wa kujiepusha na maasi, hauhusiki na watu fulani.

Ambaye Amewaumba Kutokana Na Nafsi Moja.

Mwenye Tafsir Al-manar amemnukuu Sheikh wake Muhammad Abduh akisema: "Mwenyezi Mungu ameficha kuhusu nafsi aliyomuumbia mtu na ameileta kwa tamko Nakira (linaloenea). Kwa hiyo nasi tunaiacha kama ilivyofichwa.

Pia Aya nyingine zinazomwambia mtu: "Ewe mwana Adam" haziondoi uficho huu. Wala hakuna kauli ya mkato kuwa watu wote ni watoto wa Adam. Inatosha kusihi kuwa msemo uliwahusu watu miongoni mwao wana wa Adam waliokuwa wakati wa kuteremshwa msemo huo."

Yametangulia maelezo katika kufasiri kisa cha Adam mwanzo mwanzo mwa Sura ya Baqara, akisema kwamba katika ardhi kulikuweko na aina ya watu waliokuwa katika jinsi hii wakafanya ufisadi na wakamwaga damu."

Kwa ufupi makusudio ya Sheikh Abduh ni kwamba Qur'an haithibitishi wala haikanushi kuwa Adamu ni baba wa watu wote; bali inawezekana kuweko na mababa kadhaa kwa watu, Adam akiwa mmoja wao. Na kwamba kauli ya Mwenyezi Mungu "Enyi wana Adamu."Inafahamisha kuwa wale waliokuweko wakati wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) walikuwa ni watoto wa Adam na wala haifahamishi kila aliyekuwako na atakayekuwako ni kizazi cha Adam.

Sisi tunamjibu, kwanza: Maamrisho na makatazo yaliyokuja katika Qur'an na Hadithi hayahusiki na aliyekuwepo wakati wa kutolewa, bali yanamkusanya kila aliyekuwepo na atakayekuwepo mpaka siku ya mwisho. Kwa sababu kadhia la kisharia lina- muhusu aliyepo na asiyekuwepo bila ya tofauti yoyote sawa na mfano wa kusema: "Atakayetimiza miaka ishirini basi ni lazima afanye jambo fulani. Mwenyezi Mungu anasema: "Je sikuwaagiza enyi wanaadamu kuwa msimwabudu shetani? Hakika yeye ni adui aliye wazi kwenu." (36:60)

Kauli hii inawaenea watu wote bila ya kumtoa hata mmoja, ni sawa wawepo wakati iliposemwa au la.

Pili: Maamrisho na makatazo katika Qur'an na Hadith ambayo wameelezwa wanadamu, ikiwa yanawahusu waliokuwa wakati wa Mtume (s.a.w.w.), sisi tusingelazimika nayo, na wala isingefaa sisi kuzitolea dalili juu ya hukumu yoyote mion- goni mwa hukumu za Mwenyezi Mungu.

Waislamu wote akiwemo Sheikh Abduh wanatoa hoja kwa Qur'an na Hadith za Mtume (s.a.w.w.) bali ndio msingi wa kwanza wa kurejelea wa itikadi na sharia ya kiislam kwa dharura ya dini.

Ikiwa taklifa inawahusu watu wote, basi watu wote watakuwa ni kizazi cha Adam. Kwa hiyo basi Sura ya 36 na Aya hii "Enyi wanadamu asiwafitini shetani kama alivyowatoa wazazi wenu katika pepo." (7:27). na Aya: "Na (kumbuka) Mola wake alipoleta katika wanadamu kizazi chao kutoka migongoni mwao." (7:172).
Na vile vile Aya isemayo: "Na hakika tumewatukuza wanadamu." (17:70), zote hizi zinakuwa ni ubainifu na tafsiri ya nafsi moja; na kwamba makusudio ya nafsi ni baba yetu Adam bila ya shaka yoyote.

Ama kauli ya Sheikh Muhammad Abduh kuwa kulikuweko na watu wengine kabla ya Adam iko mbali na tunayoyaeleza. Kwa sababu maneno yako katika jinsi ya viumbe iliyobaki sio jinsi iliyokwishapotea.

Zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametuambia kwa kauli yake: "Enyi watu" na "Hakika tumewaumba kwa udongo." (22:5).

Vilevile Aya: "Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu, ni kama mfano wa Adam; alimwumba kutokana na udongo," (3:59).

Aya hizi tukiziunganisha, natija itakuwa "Nyote mmetokana na Adam na Adam anatokana na udongo" kama inavyosema Hadith tukufu.

Tatu: Imethibiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w..) kwamba yeye amesema: "Mimi ni bwana mkubwa wa kizazi cha Adam." Je yuko mwislamu yeyote anayedhani tu au kufikiria kuwa Mtume alikuwa anakusudia aina maalum ya watu na sio watu wote? Swali hili hasa limwelekee Sheikh Muhammad Abduh.

Na Akamuumba Mkewe Katika Nafsi Hiyo.

Inassemekana kuwa herufi Min (katika) ni ya kuonyesha baadhi; na makusudio ni mkewe Hawa na kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu alimuumba kutokana na ubavu wa Adam. Pia imesemekana kuwa alimuumba kutokana na ziada ya udongo wa Adam, kama zielezavyo riwaya nyengine.

Ilivyo ni kuwa hakuna dalili ya kuonyesha baadhi, bali inawezekana kuwa ni ya kubainisha; mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na katika ishara zake ni kuwa amewaumbia wake zenu katika jinsi yenu. (30:21)"

Maana yake ni kuwa kila nafsi na mkewe wameumbwa katika asili moja ambayo ni mchanga kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: " Na katika ishara zake ni kuwa amewaumba kwa udongo kisha mmekuwa watu wanaoenea." (30:20)

Ama kauli ya kuwa makusudio ya mke wake ni Hawa, haina dalili yoyote kutoka kwa Qur'an ambapo haikutajwa kabisa.

Na Akaeneza Kutokana Na Hao Wawili Wanaume Wengi Na Wanawake.

Yaani na wanawake wengi pia. Haikutajwa sifa ya wengi kwa vile ile ya kwanza imefahamisha hii ya pili. Ajabu ni kauli ya Razi kwamba kwa kusifiwa wanaume kwa wingi, ni umashuhuri na kuonekana; kinyume na hali ya wanawake ambayo inakuwa ni kutokuwa mashuhuri na kufichika.

Kauli hii ya Razi inafahamisha tu kuwa amehukumia tabia ya mwanamke kulingana na desturi za jamii anayoishi.

Kimsingi ni kuwa desturi hizi hugeuka na kubadilika kutokana na wakati ulivyo. Kwa hiyo ni makosa kuchukua kipimo cha jumla kutokana na desturi maalum.

Vyovyote itakavyokuwa maana yake iko wazi, ni kwamba mtu anazaliwa kutokana na mke na mume; na kutokana na wawili wao (mke na mume) ndio mamilioni yanaenea kizazi baada ya kizazi. Inasemekana kuwa ulimwenguni hivi sasa kuna watu zaidi ya Billioni tatu1 .

Na Mcheni Mwenyezi Mungu Ambaye Kwaye Mnaombana Na Ndugu Wa Damu.

Hii ni ishara ya yale wayasemayo baadhi yetu kwa mfano 'haki ya Mungu au haki ya mama. (Kuomba mtu afanye kwa haki ya mungu au ya ndugu (kizazi))

Makusudio ya amri ya kumcha Mwenyezi Mungu na udugu wa damu ni kutekeleza haki zetu kwao. Aya iko katika mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu."Ya kwam- ba unishukuru mimi na wazazi wako…" (31:14).

Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametuamrisha katika Aya hii kuogopa ghadhabu na adhabu yake, kuwafanyia mema ndugu wa damu, tusifanyiane kibri na tusidhulumiane.

Kwa sababu wote ni wa asili moja. Amemalizia Mwenyezi Mungu kwa kusema: Hakika Mwenyezi Mungu anawachunga. Haya ni makemeo na ni kiaga kwa yule anayeasi na kung'ang'ania uasi.

وَآتُوا الْيَتَامَىٰ أَمْوَالَهُمْ ۖ وَلَا تَتَبَدَّلُوا الْخَبِيثَ بِالطَّيِّبِ ۖ وَلَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَهُمْ إِلَىٰ أَمْوَالِكُمْ ۚ إِنَّهُ كَانَ حُوبًا كَبِيرًا {2}

Na wapeni mayatima mali zao wala msibadilishe kibaya kwa kizuri. Wala msile mali zao kwa mali zenu;hakika hiyo ni dhambi kubwa.
  • 1. Hapa ni wakati wa kuandikwa kitabu, ambapo hivi sasa wakati wa kufasiri mwaka 2004, inakisiwa kuwa duniani kuna watu zaidi ya Billioni tano.