read

Aya 13 - 14: Mipaka Ya Mwenyezi Mungu

Maana

Maana yako wazi, kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) baada ya kubainisha viwango vya urithi kulingana na ujuzi wake na hekima yake, akamwahidi thawabu yule mtiifu na mateso yule mwasi; kwa kuhimiza utiifu na tishio la maasi.

Ametumia tamko la wengi (ni wenye kudumu) kwa watu wa peponi kwa vile watu wa peponi watastarehe kwa pamoja. Na kwa watu wa motoni ametumia tamko la mmoja (ni mwenye kudumu) kwa vile kila mmoja atakuwa akiteseka kivyake.

Kuna Hadith kadhaa zimepokewa kuhusu ubora wa ilimu ya mirathi (Faraidh), kwa vile inaangalia masilahi ya jamii na kumweka kila mtu na daraja yake kwa marehemu, bila ya kumnyima mwanamke wala mtoto mdogo; inaigawa mirathi yote bila kutoa nafasi ya kuilimbikiza mikononi mwa wachache; kama zilivyo baadhi ya taratibu za Kimagharibi ambazo zinamkusanyia urithi mtoto mkubwa.

Mtume (s.a.w.) amesema: "Jifundisheni ilimu ya mirathi na wafundisheni wengine, kwani mimi ni mtu nitakayekufa na kwamba ilimu - yaani sharia ya Kiislam - itazuiwa, na idhihiri fitina, mpaka itokee wawili watofautiane katika fungu wasipate atakayewaamua. Jifundisheni mirathi kwani hiyo ni katika dini yenu na kwamba kuijua ni nusu ya ilimu na ndio kitu cha kwanza kitakachowatoka umati wangu." Kauli yake hii Mtume ya mwisho (kitu cha kwanza kitakacho watoka umati wangu), ni ishara ya hizi sheria za kutungwa ambazo zimechukua mahali pa sharia ya Kiislam.

وَاللَّاتِي يَأْتِينَ الْفَاحِشَةَ مِنْ نِسَائِكُمْ فَاسْتَشْهِدُوا عَلَيْهِنَّ أَرْبَعَةً مِنْكُمْ ۖ فَإِنْ شَهِدُوا فَأَمْسِكُوهُنَّ فِي الْبُيُوتِ حَتَّىٰ يَتَوَفَّاهُنَّ الْمَوْتُ أَوْ يَجْعَلَ اللَّهُ لَهُنَّ سَبِيلًا {15}

Na ambao hufanya uchafu miongoni mwa wanawake wenu, washuhudizieni watu wane katika nyinyi. watakaposhuhudia, basi wazuilieni majumbani mpaka wafikwe na mauti au Mwenyezi Mungu awafanyie njia nyingine.

وَاللَّذَانِ يَأْتِيَانِهَا مِنْكُمْ فَآذُوهُمَا ۖ فَإِنْ تَابَا وَأَصْلَحَا فَأَعْرِضُوا عَنْهُمَا ۗ إِنَّ اللَّهَ كَانَ تَوَّابًا رَحِيمًا {16}

Na wawili ambao hufanya uchafu katika nyinyi waudhini. Na wakitubia na wakatengenea, basi waacheni. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kukubali toba mwenye kurehemu.