Aya 123 - 127: Vita Vya Badr
Mwenyezi Mungu katika Aya hizi, anawakumbusha waislamu vita vya Badr ambavyo vilimalizika kwa ushindi wa Waislamu. Badr ni kisima kilichoko baina ya Makka na Madina. Kilikuwa ni cha mtu aitwaye Badr, ndio kikaitwa jina lake.
Msafara wa kibiashara wa Makuraish ulikuwa ukipitia hapo. Waislamu wakaamua kuukatiza msafara kwa kuushambulia. Msafara huo uliongozwa na Abu Sufyan, wakatoka wapiganaji washirikina kiasi cha elfu moja, wakiwa wamejiandaa tayari kuuhami msafara huu. Hapo vita vikaumana na waislamu walikuwa 313.
Waislamu walipata ushindi mkubwa sana katika vita hivi na hasara kubwa kwa washirikina, vita hivi vilisikika Uarabuni kote. Tutarudia maelezo ya vita vya Badr Inshaallah tutakapofasiri Sura Anfal (8:7)
Maana
Hakika Mwenyezi Mungu aliwanusuru katika Badr hali nyinyi ni madhalili. Basi mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kushukuru.
Hii ni kuwakumbusha waislamu siku ya Badr kwa ajili ya taqwa ya nyoyo zao, wakati huo walikuwa wachache tena bila ya maandalizi ya nguvu. Ambapo idadi ya waislamu ilikuwa ni watu 313, wakiwa na farasi mmoja tu. washirikina walikuwa elfu moja na farasi mia moja, hata hivyo washirikina 70 waliuwawa na kutekwa 70. Waliobaki wakashindwa. Kusudio la kukumbushwa kwao haya ni kuwabainishia kwamba ushindi katika vita hauhisabiwi kuwa ndio ushindi wa mwisho, wala kushindwa katika vita hakuhisabiwi kuwa ndiko kushindwa kabisa, isipokuwa ushindi wa mwisho ni wa wenye uthabiti na wanaomcha Mwenyezi Mungu, wenye ikhlasi.
Yamefahamisha uhakika wa hilo, matukio na vita vya zamani na vya sasa; hasa vita vya pili vya dunia ambavyo vilianza mwaka 1939 na kumalizika 1945.
Ulipowaambia waumini hii ni kauli kutoka kwa Mtume (s.a.w) siku ya Badr:
Je, haiwatoshi Mola wenu kuwasaidia kwa malaika elfu tatu wenye kuteremshwa.
Yaani wenye kuteremshwa kutoka mbinguni.
Ndiyo! Kama mkisubiri na kumcha Mwenyezi Mungu, na wakawajilia katika wakati wao huu, atawasaidia Mola wenu na Malaika elfu tano walio na alama.
Dhamiri ya wakawajilia inarudia washirikina. Yaani wakiwajia tena hao washirikina, Mwenyezi Mungu atawaletea malaika. Neno Musawimina linatokana na Simau (alama). Yaani wana alama inayofahamisha.
Hakika kauli hii ya Mwenyezi Mungu imefahamisha ufahamisho usiokubali Taawili yoyote kwamba Mwenyezi Mungu, uliotukuka uwezo wake, aliwasaidia waislamu kwa Malaika katika baadhi ya vita vyao. Hadith nyingi zimefahamisha hilo.
Wameafikiana waislamu kwamba Mwenyezi Mungu aliwateremsha Malaika siku ya Badr kuwanusuru waumini, wakatofautiana kuhusu kuteremshwa kwao siku ya Uhud.
Hakuna mwenye shaka kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwateremsha Malaika siku ya Badr kwa ajili ya kuwasaidia waumini, lakini hatujui kama ulikuwa ni msaada wa kuonekana kama vile kupigana, au ni msaada usionekana kama vile kuwahofisha washirikina, na kuwapa utulivu waumini. Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi wala hatuna wajibu wowote wa kufanya utafiti na kulichunguza hilo, kwamba hata tukifanya utafiti hatuwezi kufikia kwenye yakini.
Hata hivyo ziko dalili zifahamishazo kwamba malaika huwa na sura za kibinadamu. Baadhi ya dalili hizo ni kama hizi zifuatazo:
(i) Aliyoyaelezea Mwenyezi Mungu kuhusu ugeni wa Ibrahim (a.s.); "Na wape habari kuhusu wageni wa Ibrahim, Hakika sisi tumetumwa kwa watu wenye makosa." (15:51-58)
(ii) Wageni wa Lut walioelezwa katika Sura 11:77
(iii) Kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema: "Akajifananisha kwake kwa (Sura ya) binadamu aliye kamili." (19:17)
(iv) Jibril alikuwa akimjia Mtume kwa Sura ya binadamu.
Lakini malaika kuwa na sura ya binadamu hakulazimishi kwamba wao walipigana kwa ajili ya Waislamu, bali inawezekana kuwasaidia kwa njia nyengine isiyokuwa kupigana.
Unaweza kuuliza: Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema: "Kwa hakika mimi nitawasaidia kwa malaika elfu moja watakaofuatana mfululizo." (8:9)
Kisha katika Aya hizi tunazozifasiri, ametaja elfu tatu; Aya inayofuatia hiyo akataja elfu tano moja kwa moja. Je, Mwenyezi Mungu aliwasaidia kwa elfu moja kwanza kisha elfu tatu, baadae tano na hivyo kuwa tisa?
Miongoni mwa yaliyojibiwa ni kwamba Mwenyezi Mungu aliwasaidia kwanza kwa elfu moja, kisha akaongeza elfu mbili, wakawa elfu tatu; tena akaongeza elfu mbili ikawa kwa ujumla ni elfu tano.
Mwengine amesema: Mwenyezi Mungu aliwasaidia waislamu siku ya Badr kwa malaika elfu moja. Kisha waislamu wakapata habari kwamba baadhi ya washirik- ina wanataka kuwasaidia Makuraish kwa idadi kubwa ya wapiganaji. Waislamu wakawa na hofu, na kuona taabu kwa sababu ya uchache wao. Ndipo Mwenyezi Mungu akawaahidi malaika elfu tano, ikiwa msaada utawajia Makuraish.
Lakini kama ilivyosema Aya: "… kama mkisubiri na mkamcha mungu na wakawajia katika wakati wao huu …" lakini msaada haukuwajia Makuraish. Kwa hiyo wakatosheka Waislamu na msaada wa elfu moja tu.
Na Mwenyezi Mungu hakuyajaalia ila ni bishara kwenu na ili mioyo yenu ipate kutulia.
Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewasaidia kwa malaika au aliwaahidi msaada, ili nyoyo zenu zipate utulivu kutokana na wingi wa idadi ya adui zenu na wala msikate tamaa kwa uchache wa idadi yenu.
Ili apate kuliangamiza kundi katika wale waliokufuru au awadhalilishe, warejee hali ya kuwa ni wenye kuambulia patupu.
Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwasaidia kwa malaika kuua na kuteka nyara, au awafedheheshe kwa kushindwa na waambulie patupu bila ya kuwa na tumaini la ushindi.
لَيْسَ لَكَ مِنَ الْأَمْرِ شَيْءٌ أَوْ يَتُوبَ عَلَيْهِمْ أَوْ يُعَذِّبَهُمْ فَإِنَّهُمْ ظَالِمُونَ {128}
وَلِلَّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۚ يَغْفِرُ لِمَنْ يَشَاءُ وَيُعَذِّبُ مَنْ يَشَاءُ ۚ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَحِيمٌ {129}