read

Aya 7 – 10: Wanaume Wana Fungu

MAANA

Aya nne hizi, kila moja ina mtazamo wake kama ifuatavyo:

1. Wanaume wana fungu katika walichoacha wazazi wawili na akraba, na wanawake (pia) wana fungu katika walichoacha wazazi wawili na akraba, kikiwa kidogo au kingi - fungu lililofaradhiwa.

Wazazi wawili wanafahamika; na akraba ni ndugu wa karibu wa kwa baba au mama; wakiwemo watoto, wajukuu na kuendelea chini, mababa, mababu na kuendelea juu, kaka, dada na watoto wao, ami na shangazi na wajomba, mama wadogo na watoto wao. Wake kwa waume, wakubwa kwa wadogo; iwe ni shilingi moja au mamilioni.

Kurithi wote hao ni lazima katika sharia ya kiislam, haijuzu kuikhalifu kwa namna yoyote ile kwa dalili ya kauli ya Mwenyezi Mungu: "Fungu lililofaradhiwa."

Hiyo inabatilisha yale yaliyokuwako wakati wa ujahilia, ya kuwazuwiya wanawake na wavulana wadogo wasirithi si kwa chochote isipokuwa tu, hawapandi farasi wala hawamzuwii adui. Ndipo uislam ukathibitisha haki ya mtu kurithi kwa kuangalia umbile lake la kiutu na wala sio kwa misingi ya kuwa aweza kupigana kwa upanga na kufuma mshale.
Shia wametolea dalili Aya hii katika kubatilisha Asaba waliyoithibitisha Sunni - tutafafanua punde - ambayo ni kuwarithisha wanaume na kuacha wanawake kwa sababu fulani; kama vile ikiwa marehemu ameacha binti na mtoto wa kiume wa kaka na binti wa kaka.

Hapo Sunni wanampa nusu bint, na nusu nyingine wanampa mtoto wa kiume wa kaka, lakini yule dadake hana chake ingawaje daraja ni sawa na huyu wa kiume. Au ikiwa maiti amemwacha dada, ami na shangazi … Qur'an inawarithisha wake kwa waume, na wao wanawarithisha wanaume tu.

Ama Mashia wao wanampa binti mali yote katika sura ya kwanza na ya pili. Kwa sababu yeye ndiye aliye karibu zaidi na marehemu kuliko kaka wa marehemu au mtoto wa kaka wa marehemu na zaidi kuliko ami yake.

2. Na wakati wa kugawanya watakapohudhuria wenye ukuruba na mayatima na maskini, basi wapeni nao kitu katika hiyo na waambieni maneno mazuri.

Makusudio ya wenye ukuruba ni jamaa wa karibu wa marehemu ambao wamezui- lika kupata mirathi kutokana na kuweko walio karibu zaidi kama ndugu na mtoto au ami na ndugu n.k. Msemo katika 'wapeni' unaelekezwa kwa waritihi au manaibu wao. Ni wazi kwamba waritihi huwapa sadaka hao wakiwa mafukara. Ama mayatima na masikini waliokusudiwa hapa, ni wale ambao hawana undugu na aliyekufa. Na amri ya kutoa hapa ni ya sunna na wala sio ya wajibu. Kama vile kusema: "Toeni sadaka japokuwa ubale wa tende." Hapa kutoa sadaka sio wajibu, lakini ni sunna inayotiliwa mkazo.

3. Na wachelee (waogope) wale ambao lau nao kama wangeacha nyuma yao watoto wanyonge wangewahofia. Basi na wamche Mwenyenzi Mungu na waseme kauli iliyo sawa.

Neno 'Na wachelee', ni amri inayoelekezwa kwa wasimamizi wa mayatima maana yake ni kwamba, ni juu ya msimamizi kuifanyia mali ya yatima, kama vile ambavyo angependa yeye wafanyiwe watoto wake lau kama angekuwa amekufa, "Mtenda hutendewa"

Imepokewa kutoka kwa Imam Musa bin Jafer (a.s.) Kwamba "Mwenyezi Mungu amemwandalia anayetumia vibaya mali ya yatima, mateso mara mbili. Kwanza hapa duniani, kuwa mali ya watoto wake nayo itatumiwa vibaya, Pili ni akhera, ambayo ni moto," Imam Ali (a.s.) anasema: "Yafanyieni vizuri yaliyo baada ya wenzenu, watu watayafanyia vizuri yatakayokuwa baada yenu."

4. Hakika wale ambao wanakula mali ya mayatima kwa dhuluma hakika wanakula moto matumboni mwao; na wataungua katika moto uwakao.

Makusudio ya kula moto ni kula yale yawajibishayo adhabu ya moto. Hiyo ni katika kutumia kinachosababishwa ambacho ni moto kwa maana ya sababu ambayo ni kula haramu. Imeelezwa katika Hadith kwamba mwenye adhabu kubwa zaidi kati ya watu ni kiongozi dhalimu; mwenye kula mali ya yatima na mwenye kushuhudia uongo.

يُوصِيكُمُ اللَّهُ فِي أَوْلَادِكُمْ ۖ لِلذَّكَرِ مِثْلُ حَظِّ الْأُنْثَيَيْنِ ۚ فَإِنْ كُنَّ نِسَاءً فَوْقَ اثْنَتَيْنِ فَلَهُنَّ ثُلُثَا مَا تَرَكَ ۖ وَإِنْ كَانَتْ وَاحِدَةً فَلَهَا النِّصْفُ ۚ وَلِأَبَوَيْهِ لِكُلِّ وَاحِدٍ مِنْهُمَا السُّدُسُ مِمَّا تَرَكَ إِنْ كَانَ لَهُ وَلَدٌ ۚ فَإِنْ لَمْ يَكُنْ لَهُ وَلَدٌ وَوَرِثَهُ أَبَوَاهُ فَلِأُمِّهِ الثُّلُثُ ۚ فَإِنْ كَانَ لَهُ إِخْوَةٌ فَلِأُمِّهِ السُّدُسُ ۚ مِنْ بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِي بِهَا أَوْ دَيْنٍ ۗ آبَاؤُكُمْ وَأَبْنَاؤُكُمْ لَا تَدْرُونَ أَيُّهُمْ أَقْرَبُ لَكُمْ نَفْعًا ۚ فَرِيضَةً مِنَ اللَّهِ ۗ إِنَّ اللَّهَ كَانَ عَلِيمًا حَكِيمًا {11}

Mwenyezi Mungu anawausia kwa watoto wenu; fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili. Wakiwa ni wanawake zaidi ya wawili, basi watapata theluthi mbili za ali- chokiacha (marehemu) na akiwa ni mmoja, basi atapata nusu. Na wazazi wake wawili kila mmoja atapata sudusi ya alichokiacha akiwa ana mtoto. Akiwa hana mtoto, na akarithiwa na wazazi wake wawili, basi mama yake atapata theluthi. Akiwa anao ndugu, basi mama yake atapata sudusi. Baada ya kutoa alivyousia au kulipa deni. Baba zenu na watoto wenu hamjui ni yupi katika wao aliye karibu zaidi kwa manufaa. Ni faradhi itokayo kwa Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi, mwenye hekima.

وَلَكُمْ نِصْفُ مَا تَرَكَ أَزْوَاجُكُمْ إِنْ لَمْ يَكُنْ لَهُنَّ وَلَدٌ ۚ فَإِنْ كَانَ لَهُنَّ وَلَدٌ فَلَكُمُ الرُّبُعُ مِمَّا تَرَكْنَ ۚ مِنْ بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِينَ بِهَا أَوْ دَيْنٍ ۚ وَلَهُنَّ الرُّبُعُ مِمَّا تَرَكْتُمْ إِنْ لَمْ يَكُنْ لَكُمْ وَلَدٌ ۚ فَإِنْ كَانَ لَكُمْ وَلَدٌ فَلَهُنَّ الثُّمُنُ مِمَّا تَرَكْتُمْ ۚ مِنْ بَعْدِ وَصِيَّةٍ تُوصُونَ بِهَا أَوْ دَيْنٍ ۗ وَإِنْ كَانَ رَجُلٌ يُورَثُ كَلَالَةً أَوِ امْرَأَةٌ وَلَهُ أَخٌ أَوْ أُخْتٌ فَلِكُلِّ وَاحِدٍ مِنْهُمَا السُّدُسُ ۚ فَإِنْ كَانُوا أَكْثَرَ مِنْ ذَٰلِكَ فَهُمْ شُرَكَاءُ فِي الثُّلُثِ ۚ مِنْ بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصَىٰ بِهَا أَوْ دَيْنٍ غَيْرَ مُضَارٍّ ۚ وَصِيَّةً مِنَ اللَّهِ ۗ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَلِيمٌ {12}

Nanyi mtapata nusu ya walichokiacha wake zenu ikiwa hawana watoto. Ikiwa wana watoto; basi mtapata robo ya walichokiacha baada ya kutoa walivyousia au kulipa deni. Na wao watapata robo ya mlichokiacha ikiwa hamna mtoto. Ikiwa mna mtoto, basi watapata thumni ya mlichokiacha, baada ya kutoa mlivyousia au kulipa deni. Ikiwa mwanamume au mwanamke anayerithiwa ni mkiwa naye ana ndugu wa kike au wa kiume, basi kila mmoja katika wao atapata sudusi. Wakiwa wengi zaidi ya hivyo, basi watashirikiana katika theluthi, baada ya kutoa yaliyousiwa au kulipa deni, pasi na kuleta dhara. Ni wasia utokao kwa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mpole.