Aya 118 - 120: Wasiri Waovu
Maana
Katika Aya zilizotangulia, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amezungumzia kuhusu watu wa Kitabu, washirikina na wenye kurtadi ambao walikufuru baada ya kuamini kwao. Wote hao amewapa kiaga na akawapa hoja, kisha akaamrisha waislamu wamche Mwenyezi Mungu, washikamane na kamba yake na waamrishe mema. Baada ya yote hayo, sasa anawahadharisha waislamu wajiepushe na makafiri - ambao wanawadhamiria uovu waislamu na kuwatakia maangamizi - kwa kusema:
Enyi ambao mmeamini! Msiwafanye wasiri wasiokuwa katika nyinyi.
Hili kwa dhahiri ni katazo kwa waislamu kwa kila asiyekuwa katika dini yao bila ya kumvua yeyote. Hapo basi litakuja Swali hili:
Ni maarufu kuwa viongozi wa dini katika mataifa yote wanaeneza kwa wafuasi wao roho ya uadui na ubaguzi, dhidi ya dini nyingine. Na hii Qur'an nayo inakwenda njia hiyo hiyo, ambapo inawaamrisha waumini kujitenga na wengine na kutoa tahadhari ya kuwafanya marafiki. Sasa kuko wapi kuvumiliana katika Uislamu? Je, kuna tofauti gani baina ya waislamu na mayahudi walioambiana: "Wala msimwamini ila mwenye kufuata dini yenu?"3:73
Jibu: Aya haikuwatahadharisha Waislamu kujiepusha na wasiokuwa wao kwa kuwa si wafuasi; isipokuwa imewahadharisha na wale wanaowafanyia vitimbi. Hayo ndiyo maana wazi ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
Hawazembei kuwaharibia; yaani wanajitahidi bila ya kufanya uzembe katika kuwadhuru na kuharibu mambo yenu. Na katika kauli yake: Wanapendelea yanayowapa mashaka.
Pia kauli yake Mwenyezi Mungu: Imedhihiri Yaani kuitia ila dini yenu, Mtume wenu na Qur'an yenu. Na wayafichayo vifuani mwao ni makubwa kuliko yale yamiminikayo kwenye ndimi zao.
Vile vile miongoni mwa sifa za wale aliowahadharisha Mwenyezi Mungu ni: wanapokuwa faragha huwaumia vidole kwa hasira. Na ukiwagusa wema unawasononesha na kama likiwapata baya wanalifurahia.
Sifa zote hizi, ndio sababu ziwajibishayo kuwakataza kuwafanya wasiri wenu. Kwa hiyo basi, kila mwenye sifa hizi ni wajibu kujitenga naye wala haijuzu kumfanya msiri; ni sawa awe ni mwislamu au si mwislamu.
Hivi sasa tuko katika mwaka 1967. Mnamo tarehe 5 Juni mwaka huu, ukoloni umeileta Israel kufanya uadui katika ardhi za Waarabu baada ya kufagiliwa njia na makombamwiko waovu wanaonasibika na dini ya waislamu na kabila ya Waarabu. Na waovu hawa mbele ya Mwenyezi Mungu wana hatia kubwa kuliko walahidi na washirikina ambao hawawaudhi wengine.
Kwa hiyo suala hapa ni la ushari na hiyana, sio suala la ukafiri na kukosa imani. Unaweza kuuliza: Ingawa mambo ni hivyo, kwa nini Mwenyezi Mungu amesema, 'wasiokuwa katika nyinyi,' badala ya kusema katika wahaini walio wafisadi?
Jibu: Aya ilishuka kwa sababu ya baadhi ya waislamu waliokuwa wakiungana na mayahudi kama walivyosema wafasiri. Kimsingi cha kuzingatia ni sababu iliyowa- jibisha sharia ya hukumu; sio sababu ya kushuka kwake. Kwa maneno mengine, ni kwamba hukumu itafuata dhahiri ya tamko, ikiwa hatujui sababu ya kushuka kwake. Ama tukiwa na yakini ya sababu yake basi hukumu itafuatia sababu, sio dhahiri ya tamko.
Tumewabainishia ishara ikiwa nyinyi ni wenye akili.
Makusudio ya neno ishara ni alama zinazo pambanua baina ya anayefaa kufany- wa msiri, na habithi ambaye ni wajibu kujitenga naye.
Hivyo basi! Nyinyi ndio hao muwapendao hali wao hawawapendi.
Dhahiri ya msemo ni kuwa unaelekezwa kwa kikundi kinachojinasibisha na uislam, wala hauswihi kuelekezwa kwa waislamu wote, si katika wakati wa mwanzo wala mwengineo. Kwani haikutokea hata siku moja kwamba waislamu waafikiane kuwapenda makafiri.
Sheikh wa wafasiri Tabari amesema na akafuatwa na wengi, kwamba waislamu kuwapenda wanaowachukia katika makafiri ni dalili kwamba uislam ni dini ya upendo na kuvumiliana. Huku ni kusahau kwa Tabari na akafuatwa na wengi, kwamba uislamu kabisa hauvumilii ufisadi na uhaini.
Tuonavyo sisi ni kwamba suala sio la kuvumiliana, isipokuwa ni suala la hiyana na unafiki kutoka kwa baadhi ya wanaojinasibisha na uislamu, na wakati huo huo wakifanya ujasusi kwa waislamu kwa ajili ya maadui wa nchi na dini. Kama wafanyavyo leo vibaraka wa ukoloni wanaojulikana kwa jina la kikosi cha tano1 askari wa kukodiwa n.k. Kwa sababu, wanauza dini yao na nchi yao kwa kila anayewapa pesa tu.
Nanyi mwaviamini vitabu vyote.
Herufi Alif na lam hapa ni ya jinsi; yaani mwamini kila kitabu kilichoteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ni sawa kiwe kimeteremshwa kwao au la. Nyinyi si kama wao wanaamini baadhi na kukanusha baadhi nyingine.
Na wakikutana nanyi husema tumeamini kwa ria na unafiki.
Haifai kwa mumin kufanya urafiki na mnafiki na mwenye ria (kujionyesha).
Na wanapokuwa faraghani huwaumia vidole kwa hasira.
Kuwaumia vidole ni fumbo la chuki zao na ukorofi wao kwenu. Hakuna kitu kinachomkasirisha adui kuliko fadhila na hulka njema, vile vile umoja na kupatana kwa undugu. Tangu zamani hadi sasa adui anajaribu kuwatawanya waislamu na umoja wao.
Sema: Kufeni na hasira zenu.
Huu ni msemo wa kiarabu kwa mtu wanayamuombea abaki hivyo: Kama kusema; 'Kufa na ugonjwa wako.' Yaani Mwenyezi Mungu akubakishe na ugonjwa wako.
Kimsingi ni kwamba maneno haya huambiwa adui akiwa msemaji ana nguvu. Na hakuna nguvu kama umoja na kuungana.
Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa yaliyo vifuani kila yanayompitia mtu na anayowazia moyoni mwake katika misukumo ya kheri na shari. Yaani Mwenyezi Mungu anajua chuki na ukorofi wao.
Ukiwagusa wema unawasononesha na kama likiwapata baya wanalifurahia.
Hiyo ni kawaida ya kila adui. Wafasiri wanasema, kumetajwa kugusa katika wema kwa kutambulisha kuwa kheri ndogo tu aipatayo Mwislamu, humsononesha adui. Na kumetajwa kupata katika uovu, kufahamisha kuwa kukiwa na baya kwa waislamu, basi maadui huzidi furaha. Huu ni ufasaha wa kuelezea uadui ulivyo mkub- wa.
Na mkisubiri kwa twaa ya Mwenyezi Mungu na maudhi ya adui zake na mkaogopa yaliyoharamishwa, na maasi, basi hila zao hazitawadhuru kitu. Anayekuwa na Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu huwa naye, na anayemcha Mwenyezi Mungu humpatia njia.
وَإِذْ غَدَوْتَ مِنْ أَهْلِكَ تُبَوِّئُ الْمُؤْمِنِينَ مَقَاعِدَ لِلْقِتَالِ ۗ وَاللَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ {121}
- 1. Franco aliposhambulia Madrid 1936 - 1939 alikuwa na vikosi vinne cha tano kilikuwa kiko ndani ya nchi kikiwasiliana nao. Kwa hivyo ikiwa kila genge linalomtumikia adui ndani ya nchi linaitwa jina hilo.(Fifth column)